|

KIFO CHA NGWEA... MAPYA YAIBUKA!

HUKU mwili wake ukitarajiwa kuwasili Bongo kesho, kifo chake Albert Mangweha ‘Ngwea’ kilichotokea katika hali ya utata Mei 28, 2013 nchini Afrika Kusini, kimeibua mambo mapya, Ijumaa Wikienda lina mzigo wote.
MAMA MANGWEA NAYE AZIDIWA, AKIMBIZWA HOSPITALI YA MKOA
Habari kutoka msibani Moro jana zilisema mama mzazi wa marehemu Mangwea, Denisia Mangwea naye alizidiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa baadhi ya waombolezaji msibani hapo, mama huyo alipata mshtuko wa moyo kufuatia kifo cha mwanaye ambapo taarifa za kifo hicho zilimshtua tangu Jumanne mpaka alipozidiwa jana. 
HABARI KUTOKA SAUZI SASA
Habari kutoka kwenye Jiji la Johannesburg ambako Ngwea alifia, mtiririko wa maelezo ya wenyeji wa Mangwea na Mgaza Pembe ‘M 2 The P’ nayo yanaibua mapya ambayo awali yalikuwa hayajulikani.

MAELEZO YA SAUTI ZA WENYEJI
Wakizungumza hewani kupitia redio moja ya jijini Dar, wenyeji wao wawili waliojitambulisha kwa jina moja moja la Godfrey na Godluck ambao walikuwa na Mangwea na M 2 The P, kila mmoja alisema lake huku maelezo yao yakionesha dalili ya kutofautiana au kuzua maswali masikioni mwa watu.

KUMBE WALITOKA
KLABU SALAMA
Godluck siku hiyo aliwaendesha wawili hao kutoka klabu kurudi nyumbani walikofikia kwa wiki mbili nyuma ambako ni kwa Godfrey. Godluck alikuwa akitumia gari lake.
Kwa mujibu wa Godluck, waliondoka klabu alfajiri kurudi nyumbani kwa Godfrey au God wakiwa salama salimini. Waligonga mlango, God akatoka kufungua, wakaigia ndani wote.
Godluck anaishi sehemu tofauti na nyumba hiyo, lakini kwa sababu saa 2:00 asubuhi Ngwea na M 2 The P walitakiwa kurejea Bongo na ni yeye ndiye aliyetakiwa kuwapeleka uwanja wa ndege, hivyo aliamua kulala palepale.
Alisema wakiwa chumbani, watu wanne, yeye, Ngwea, M 2 The P na mwenyeji Godfery, Ngwea alianza kuonesha dalili za kushangaza.
“Kule chumbani Ngwea alikuwa ananilalialalia huku amelegea, nikawa namuuliza we vipi? Hanijibu, mara akanitapikia, nikamwamsha hakuamka, nikamwamsha God (Godfrey) na kuuliza huyu vipi? Nikamwamsha M 2 The P, nikamuuliza huyu vipi, mbona ananitapikia, akasema huyo ndiyo zake akilewa huwa anakuwa hivyo, si unajua mambo yake tena,” alisema Godluck akikariri maneno ya M 2 The P.
Aliendelea kusema kuwa ghafla alimuona M 2 The P naye kama akaanza kuzidiwa. “Nikamuuliza we vipi? Lakini nikajua labda ni haya mambo yao, maana unajua mimi nilikuwa siwaelewielewi,” alisema Godluck.
Alisema ilipofika saa mbili asubuhi, akiwa anajua wasafiri hao wameshachelewa ndege, yeye aliamua kuondoka kurudi kwake ambako si mbali akipanga kwenda kulala hadi mchana.
Akasema: Lakini nikiwa nakwenda nyumbani, NILIMPIGIA SIMU MIDO, dogo mmoja anaishi jirani, nikamwambia wale jamaa (akina Ngwea) kama wamezidiwa, nenda kawacheki.
Alisema akiwa amelala, aliamshwa na simu ya Mido, akaipokea na kuambiwa hali za jamaa hao ni mbaya sana hivyo yeye akalazimika kwenda na kuwapakia kwenye gari lake WOTE WAWILI hadi Hospitali ya St. Hellen Joseph  ambako ilithibitishwa na daktari kwamba, Ngwea aliaga dunia ila M 2 The P hali  tete.

MAELEZO YA GODFREY SASA
“Siku ya mwisho, walitoka wakarudi asubuhi, wakanigongea mlango, nikawafungulia. Wakaingia, Ngwea akaniambia NICHUKUE ‘KONTAKTI’ (mawasiliano) yake, nikachukua notebook yangu na kuandika. Walikuwa wazima kabisa.
“Basi, tukawa tunaongeaongea pale kama mtu wa kawaida tu. Hakuniambia kama anaumwa popote wala hakula chochote.
“Baadaye ndiyo wote wawili wakazidiwa, tukawachukua kuwapeleka hospitali ambako daktari alisema Ngwea alifariki dunia lakini M 2 The P hali yake ilikuwa mbaya akalazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).”

KUNA MADAI MAITI YA
NGWEA ILITUPWA NJE YA JIJI
Mtangazaji alimuuliza Godfrey kuhusu madai kwamba, kabla ya Ngwea kupelekwa hospitalini, mwili wake ulikutwa nje ya Jiji la Johannesburg ukiwa umetupwa.
Godfrey: Si kweli, alizidiwa palepale nyumbani ndiyo tukamchukua kumpeleka hosptali. NGWEA NILIMPAKIZA KWENYE GARI LANGU, mwenzake alikuwa kwenye gari la nyuma.

MASWALI MAGUMU
Katika maelezo ya wawili hao, Godluck alisema alipokuwa anarudi kwake, alimpigia simu dogo anaitwa Mido na kumwambia kuhusu kuzidiwa kwa akina Ngwea aende akawacheki, kwa nini asimpigie simu Godfrey ambaye ndiye mwenyeji wa wawili hao, ndiye aliyewafungulia mlango na ndiye aliyemwamsha  kumwambia kuhusu hali ya Ngwea?
Godluck yeye alisema aliwapakia wawili hao kwenye gari lake hadi hospitali, lakini Godfrey alisema alimpakia Ngwea kwenye gari lake na M 2 The P alipakiwa kwenye gari jingine la nyuma yake (labda la Godluck).
Godfrey, kwa mtangazaji alikiri kuishi na Ngwea kwa wiki mbili, lakini pia akasema usiku wa kuamkia kifo chake marehemu alimpa mawasiliano, ina maana hakuwa na kontakti za Ngwea kwa siku zote kumi na nne alizoishi pale?

MANENO YA MAMA YAKE MZAZI
Jumamosi iliyopita, mwandishi wetu mkoani Morogoro alifika msibani na kufanikiwa kukutana na mama mzazi wa Ngwea, Denisia Mangwea akiwa na majonzi mazito ambapo alisema:
“Mwanangu Albert amekwenda, najua sitamuona tena katika maisha ya duniani, inaniuma sana. Nilimpenda sana na yeye alinipenda sana lakini Mungu kaamua kumchukua.”

MAZIKO
Kumekuwa na utata wa kuwasili kwa mwili wa marehemu Ngwea, awali ilidaiwa ungefika jana na kuzikwa Jumanne, Kihonda Morogoro, lakini baadaye ikadaiwa mwili huo sasa utawasili kesho Jumanne.
Wakati hayo yakiendelea, jana Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya alikwenda nyumbani kwa baba mdogo wa marehemu Ngwea, David Mangwea, Mbezi Beach, Dar na kusaini kitabu cha maombolezo.
MUNGU ailaze pema peponi roho ya marehemu Mangweha. Amina.
chanzo:globalpublishers.

Posted by Unknown on 1:53 AM. Filed under , , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for "KIFO CHA NGWEA... MAPYA YAIBUKA!"

Leave a reply