|

TUHUMA NZITO: WABUNGE BONGO WANAJICHUBUA!

KUMBE! Baadhi ya wabunge wa kike ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanatumia vipodozi vinavyochubua ngozi ya juu ya mwili ili wawe na mwonekano mweupe (kama wazungu).
Kauli hiyo ya kushangaza ilitolewa bungni Mei 9, mwaka huu na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy wakati alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu udhibiti wa dawa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Akizungumza bila kupepesa macho, Mheshimiwa Kessy  alisema kuwa baadhi ya waheshimiwa wa kike ndani ya mjengo wanatumia vipodozi ambavyo vina madhara makubwa kwa afya ya mtumiaji.

MSIKILIZE KWA KINA
“Labda niseme tu TFDA wanapaswa kusimamia kuhakikisha vipodozi vyenye madhara haviingii nchini, watu wengi sana wanaathirika na kupata magonjwa ya kansa ya ngozi.
“Humu ndani (bungeni) wapo waheshimiwa ambao wanatumia vipodozi hivyo ambapo wanapokuja kuumwa serikali inapoteza fedha nyingi kwenda kuwatibia nje ya nchi,” alisema Kessy.
WABUNGE WAMEKASIRIKA?
Habari za ndani zinaweka wazi kwamba, baada ya Mheshimiwa Kessy kuzungumza madai hayo, baadhi ya waheshimiwa hao wameonesha kukasirishwa na kauli hiyo wakisema ililenga kuwachafua.
“Kwa kweli waheshimiwa wangekuwa wanachuja cha kuzungumza, mambo mengine ukiyasikia unapata picha kwamba lengo la msemaji ni kuchafua watu,” aliweka wazi mbunge mmoja alipoongea na gazeti hili huku akigoma jina lake lisiandikwe gazetini.
ALICHOSEMA MTAALAM WA AFYA
Baada ya kauli hiyo ya Mheshimiwa Kessy ambayo ndiyo habari ya mjini kwa sasa, Ijumaa Wikienda lilizungumza na mtaalam wa masuala ya afya ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Alibainisha kuwa tatizo litokanalo na matumizi ya vipodozi vikali ni kubwa sana Bongo na kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele, taifa linazidi kuangamia kwa ugonjwa wa kansa ambayo husababishwa na kujichubua.
“Serikali kupita mamlaka zinazohusika inapaswa kutilia mkazo suala hili na kuhakikisha inathibiti mianya yote ya kuingizia madawa haya ambayo madhara yake ni makubwa kwa taifa, hasa magonjwa ya ngozi kama vile kansa.
“Hii ni hatari kubwa sana, kwa sababu wabunge ambao ndiyo walipaswa kuwa mfano wa kuigwa, badala yake wao wenyewe wanadaiwa kuwa watumiaji wazuri,” alisema mtaalam huyo
chanzo:.globalpublishers

Posted by Unknown on 5:07 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for "TUHUMA NZITO: WABUNGE BONGO WANAJICHUBUA!"

Leave a reply