|

Mtoto wa miezi miwili anajisiwam, atokwa na kinyesi bila kikomo.


Mpwapwa. Katika miaka ya hivi karibuni  kumeibuka habari kuhusu ukatili unaofanywa dhidi ya watoto. Hii siyo tena jambo la ajabu.
Baadhi ya ukatili huo ni pamoja na kubakwa na ule wa kukatwa viungo vya mwili kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Licha ya kupigiwa kelele, hata kampeni mbalimbali za kupinga kufanyika, unyama huo umeendelea kufanyika na tukio la hivi karibuni limemhusisha mtoto  Erisia Tito mwenye miezi miwili  anayedaiwa kunajisiwa wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
Tukio hilo limekuwa gumzo katika mitaa mbalimbali wilayani humo, huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa linahusiana na imani za kishirikina.
Unaweza kujiuliza maswali mengi, hata inakuwaje mtoto wa miezi miwili kunajisiwa?
Katika vijiwe vya kahawa wilayani Mpwapwa, hii ni habari kubwa zilizokuwa zikizungumzwa   kuhusu kunajisiwa kwa mtoto huyo swali likibaki;  Je, yule mtu alimnajisi mtoto ameishia wapi?
Naingia chumba cha Mganga Mkuu Wilaya ya Mpwapwa kupata maelezo ya mtoto huyo tangu alipofikishwa katika hospitali ya wilaya hiyo, maendeleo yaliyofikiwa na utaratibu wa kiuchunguzi unavyoendelea.
Kauli ya Mganga Mkuu
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Lunemo Sakafu anasema kuwa tangu alipolazwa, mtoto huyo alikuwa akipelekwa kliniki kwa ajili ya kupatiwa chanzo mbalimbali na kupima afya yake, kwamba alikuwa na afya nzuri.
“Hakuzaliwa katika hospitali hii ila alikuwa akihudhuria kliniki, alizaliwa kwa wakunga wa jadi na mara ya mwisho kuja hapa hospitali ilikuwa Aprili 15, mwaka huu na alikuwa na afya nzuri,” alisema
Ashangazwa
Alisema kuwa alishangazwa na hali aliyokuwa nayo mtoto huyo alipofikishwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo kwani alikuwa akitokwa haja zote bila kikomo.
“Tunampatia matibabu ya kina ili kujua tatizo ni nini. Kwa sasa tuna utaratibu wa kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ili akafanyiwe vipimo vya kina kwa kuwa mtoto huyu anatoa haja zote bila kikomo,” anasema  Sakafu.
Kauli za wazazi
Baba wa mtoto huyo, Silvani Msemakweli anasema kuwa tangu mtoto wake alipozaliwa alikuwa na maumivu wakati wa kupata haja kubwa.
“Tangu alipozaliwa hali hii ilikuwapo hasa wakati wa kujisaidia haja kubwa mtoto analia, kwani husikia maumivu makali. Katika ukoo wetu yupo mmoja wa ndugu zetu aliyewahi kuwa na mtoto aliyekumbwa na hali kama hii ya mtoto wangu,” anasema na kuongeza:
“Yeye alipona baada ya kutumia dawa za kienyeji na alipona kabisa, siyo kweli kuwa mtoto alinajisiwa.”
Msemakweli anaongeza kuwa ni vigumu kuamini kama mtoto huyo amenajisiwa kutokana na mazingira ya familia hizo mbili, yaani familia yake na ya mke wake.
“Japo sikuwapo siku hiyo, lakini bado siamini kama mtoto wangu atakuwa amenajisiwa. Kwa sasa mama yangu ndiyo anayeshikiliwa na polisi na kufunguliwa kesi,” anasema Msemakweli.
Mama wa mtoto huyo, Rejina Msemakweli anasema kuwa yeye alijifungua kwa mkunga wa jadi aliyemtaja kwa jina la Hilda Maderemo na kwamba mtoto alikuwa mzima na hakuwa na tatizo lolote.
Anasema kuwa baada ya kujifungua alianza kumpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kwa ajili ya kupata chanjo mbalimbali.
“Mwanangu nilimzaa akiwa mzima nilishangaa siku moja analia sana wakati huo alikuwa amepakatwa na bibi yake,” anasema na anaongeza:
“Nilimwacha na bibi yake kwa kuwa nilikwenda shambani ila niliporudi nilimkuta akiwa analia kupita kiasi. Nilimchukua na kumwogesha, lakini kabla sijamaliza niligundua kuwa ameumia sehemu zake za siri na alikuwa akitoka kinyesi mfululizo, yaani mbele na nyuma.”
Regina anaeleza kuwa familia yake ina watoto wawili ambao wote ni wasichana, mume wake pamoja na mdogo wake wa kike, kwamba pia wanaishi kwa ukaribu mkubwa na familia ya mume wake.
“Katika maisha yetu nimekuwa nikiishi na wakwe zangu bila maelewano mazuri, familia imekuwa ni yenye kugombana kila wakati, hata kama kitu ni kidogo. Lakini yataibuka mambo makubwa kiasi kwamba utadhani ni watu wasio familia moja inaniuma sana,” alisikitisha.
“Naongea kwa kuvumilia tu, lakini moyoni ninaumia kwa kiasi kikubwa kuona mwanangu amekuwa katika hali kama hii sielewi. Tukijaribu kumwuliza mama mkwe wangu hasemi ukweli kuwa mtoto amekuwaje,” anasimulia Regina huku akilia machozi.
Anasema kuwa aligundua kwamba sehemu za siri za mtoto wake zimevimba na kuonyesha kukwaruzika huku akitokwa na kinyesi bila kikomo.
Kauli ya mkunga
Mkunga Hilda Mademo anakiri kuwa alimzalisha Regina na kwamba mtoto huyo alikuwa mzima bila kuwa na kasoro yoyote.
“Mimi ndiye niliyemzalisha mama huyo na mtoto alizaliwa akiwa mzima kabisa. Suala la kupatikana kwa tatizo hilo, ukweli wanao wazazi wenyewe. Huduma zangu nilizitoa hata hospitali ya wilaya inalifahamu, walinitembelea hadi hapa kuona mazingira ninayofanyia kazi na kunisaidia baadhi ya vifaa kwa mfano haya mabakuli,” anasema Hilda.
Polisi yatoa tamko
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi David Misime anakiri kupokea taarifa za kunajisiwa kwa mtoto wa miezi miwili katika Kijiji cha Ising’u wilayani Mpwapwa.
“Sisi tulipokea taarifa hiyo na kuanza kuifanyia kazi za awali, hadi sasa bibi wa mtoto huyo yuko mikononi mwa polisi.  Tunasubiri jibu la kitaalamu kutoka kwa daktari kwa kuwa wakati mtoto amepelekwa katika hospitali,”alisema Misime na kuongeza:
“Katika Kituo cha Polisi hapakuwa na ushahidi wa kujitosheleza kwa kuwa mtoto huyo tayari alikwishasafishwa siku tatu zilizopita.”
Viongozi wa Serikali wakemea
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, Ryoba Kangoye amekemea vikali tukio hilo na kuliita ni la ugaidi kwa kuwa mtu huyo hakuwa na nia ya kubaka bali ni kuua.
“Hii hali siyo ya kawaida ni mstuko mkubwa kusikia hili kama hiyo kujitokeza katika mazingira hayo. Hivi, Mtanzania wa leo kufikia kufanya jambo kama hilo ni ajabu kubwa, hata hiyo familia kukaa kimya ni kunyima haki vyombo vya sheria kufanya kazi zake na kupoteza ushahidi uliokamika,“ anasema Kangoye.
Mtendaji wa kijiji hicho, Emmanuel Mamba anasema kuwa waliposikia tukio hilo walijikuta ni kama wamemwagiwa maji au tindikali wakilifananisha na mauaji.
“Tulioposikia tuliishiwa na nguvu kwa kuwa hata kama matendo kama hayo hufanyika, basi isingekuwa kwa mtoto mdogo kama huyo, asiye na uwezo wowote ule. Tulijiuliza maswali mengi hata kuhisi huenda walitaka kumfanyia ukeketaji,” anasema Mamba
Viongozi wa dini
Kwa niaba ya madhebu ya dini, Padiri Masasi Deo kutoka Kanisa la Katoliki Mpwapwa, amekemea vikali tabia hiyo akisema:
“Nionavyo sasa umefika wakati wa watu wenye dhamana na jamii kukaa pamoja na kufanya ibada na kujua mbinu mpya ya kufundisha maadili kutokana na hali ya maadili ilivyobadilika nchini.”
Haki za binadamu
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu (AFNET)Mkoa wa Dodoma, Sara Mwanga amesema kuwa kitendo hiko ni unyama na kwamba jamii bado haina elimu ya kujitambua kuhusu ukatili unaofanywa hasa katika kushughulikia kesi za aina hiyo.
chanzo:mwananchi

Posted by Unknown on 5:21 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0. Feel free to leave a response

0 comments for " Mtoto wa miezi miwili anajisiwam, atokwa na kinyesi bila kikomo. "

Leave a reply